Bajeti ya tano ya mweka hazina wajimbo hilo Cameron Dick, ita tolewa hii leo na inatarajiwa kusimamishwa kwa ada na malipo ya serikali, yatakayo jumuisha gharama za leseni za kuendesha gari, jumla yake ikiwa $180 milioni kwa mwaka wa fedha wa 2024/25. Hii ni sehemu ya juhudi pana yakutoa afueni kufuatia makubaliano ya $8.224 bilioni mwaka jana. Familia zote zitapokea $1,000 kwa bili za nishati kutoka serikali ya jimbo mwaka ujao, na $300 za ziada kutoka serikali ya madola.
Kiongozi wa jimbo la New South Wales Chris Minns amesema bajeti ijayo ya jimbo hilo itajumuisha $15.1 milioni zakupunguza shinikizo kwa idara za dharura. Uwekezaji huo unatarajiwa kutumiwa kuboresha mifumo ya afya ya umma ya ugawaji wa wagonjwa wa gari za wagonja. Bajeti hiyo itazingatia uwezo wa idara za dharura za karibu, muda wakusafiri pamoja na hali ya mgonjwa kupitia data itakayo changiwa mubashara. Serikali ya jimbo tayari imetangaza mpango wa $480 milioni, wakuboresha idara za dharura za hospitali.
Waziri wa afya wa shirikisho amesema anafuatilia kwa karibu uwezekano wa hatari kwa binadam wa mlipuko wa mafua ya ndege jimboni Victoria. Mark Butler amesema usimamizi wa mlipuko wa H-7-N-3 katika shamba la mayai inatia moyo na jimbo hilo linafanya kazi kwa karibu na serikali ya madola. Ila amekiri mamlaka daima wako waangalifu kwa uwezekano wa maambukizi kwa binadam. Bw Butler amesema kukabiliana na mafua ya ndege ni tatizo la dunia, kila bara isipokuwa Australia kwa sasa inakabiliana na milipuko ya aina ya virusi vya H-5-9-1. Kufikia sasa zaidi ya kuku nusu milioni wame angamizwa jimboni Victoria, wakati masoko ya Coles yame weka vikomo vya katoni mbili kwa wateja wanao nunu mayai kote nchini isipokuwa Magharibi Australia. Waziri huyo amejiunga na viongozi wenza, kuwa sihi wateja wasi anze kununua bidhaa kwa woga.
Takriban wanaume wawili hupotezwa kila saa kwa vifo ambavyo vinaweza zuilika nchini Australia. Sababu kuu ya kifo ya wanaume 50 kila siku ni ugonjwa wa moyo ila, kongamano la Afya ya Wanaume wa Australia ime onya kuwa kudumisha uhai wa wanaume kwa muda mrefu zaidi, unahusu mengi zaidi kuliko afya ya mwili. Kujiuwa ni moja ya sababu kubwa kwa wanaume wenye chini ya miaka 55, takriban nusu ya wanaume wote wakipitia aina fulani ya uzoefu wa ugonjwa wa afya ya akili katika maisha yao. Jana jumatatu wafanyakazi wa huduma za dharura wa shirika la Ambulance Victoria, wameomba wanaume na marafiki wao wafanyiwe vipimo vya afya, hiyo ilikuwa mwanzo wa wiki yakimataifa ya Afya ya wanaume.
Vyama vya Afrika Kusini Jumatatu hii vinajadili mpango wa kuunda serikali ya mseto huku Rais Cyril Ramaphosa akitoa wito kwa vyama vyote kufanya kazi kwa pamoja. Chama cha Ramaphosa cha African National Congress (ANC) kilipata asilimia 40 ya kura , kiwango cha chini zaidi kuwahi kutokea tangu kuanza kwa demokrasia mwaka 1994, na sasa kinahitaji kuungwa mkono na vyama vingine ili kutawala. Chama cha ANC tayari kimedokeza kinataka kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kundi pana la vyama vya upinzani, kuanzia mrengo wa kulia hadi mrengo mkali wa kushoto.
Wadau wa siasa nchini Tanzania bado wanalalamikia mapungufu yaliyojitokeza katika sheria za uchaguzi zilizopitishwa hivi karibuni na bunge la taifa hilo la Afrika Mashariki.
Wadau hao pamoja na mambo mengine wameisisitiza serikali ya nchi hiyo kuwa na uchaguzi mmoja, utakaojumuisha serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. Wadau wa siasa wakiongozwa na Jukwaa la Katiba Tanzania,JUKATA wamesema hayo Jumatatu walipokutana na wanahabari jijini Dar es Salaam, na kubainisha kuwa, wanaishinikiza serikali ifanye mabadiliko ya katiba kwani kufanya chaguzi mbili tofauti, wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu, mwaka 2025, ni kuingia gharama zisizo na msingi.
Polisi wa Kenya watapelekwa nchini Haiti kukabiliana na magenge ya uhalifu pengine ndani ya wiki zijazo, rais wa Kenya William Ruto alisema Jumapili, licha ya pingamizi za mahakama ambazo zilichelewesha mchakato huo. Kenya imekubali kuongoza kikosi kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kulinda taifa hilo la Caribbean, linalokumbwa na machafuko, umaskini na ukosefu wa uthabiti wa kisiasa. Taifa hilo la Afrika mashariki linapanga kupeleka maafisa 1,000 wa polisi kwa ajili ya operesheni hiyo pamoja na polisi wengine kutoka nchi nyingine kadhaa. Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Oktoba mwaka jana liliidhinisha kupelekwa kwa kikosi hicho lakini mahakama ya Kenya mwezi Januari ilichelewesha mchakato huo.